TUME YA TAIFA ya Uchaguzi
nchini Rwanda imetangaza orodha ya muda ya wagombea urais katika uchaguzi
utakaofanyika mwezi ujao. Rais Paul Kagame atachuana na wapinzani wawili
wanaoonekana kutokuwa na ushawishi mkubwa.
Mkuu wa Tume hiyo ya
Taifa ya Uchaguzi Oda Gasinzigwa ametangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa
walipokea jumla ya maombi tisa ya wagombea kiti cha urais, lakini orodha ya
muda baada ya mchujo imewaidhinisha wagombea watatu katika uchaguzi wa Julai 15
kuwa Paul Kagame wa chama tawala cha RPF, Frank
Habineza wa Democratic Green Party na mgombea huru Philippe Mpayimana.
Itakumbukukwa kuwa
Habineza na Mpayimana walikuwa pia wagombea pekee walioidhinishwa kuchuana na
Kagame katika uchaguzi wa mwaka 2017 ambao wote hao wawili hawakuweza hata
kupata asilimia moja ya kura. Orodha ya mwisho ya wagombea ikitarajiwa
kutangazwa Juni 14.
Mpinzani na mkosoaji wa
Kagame azuiliwa kugombea
Jina la Diane Rwigara
kiongozi wa chama cha People Salvation Movement ambaye pia ni mgombea maarufu
zaidi wa upinzani na mkosoaji wa wazi wa utawala wa Kagame limeondolewa kwenye
orodha hiyo kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.
Alipotangaza rasmi nia
yake ya kugombea urais mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Bi Rwigara mwenye umri
wa miaka 42 alikuwa na matumaini:
"Ninapolinganisha
changamoto zilizojitokeza mwaka 2017 na zinazoshuhudiwa mwaka huu, naweza
kusema ilikuwa vigumu zaidi miaka saba iliyopita. Kwa hivyo ni mabadiliko
mazuri na ninatumai hali itaendelea hivi. Lakini haimaanishi kuwa hatujakutana
na changamoto zozote, lakini ninapolinganisha na mapambano yetu ya mwaka 2017,
naweza kusema kuwa mwaka huu ilikuwa rahisi zaidi."
Tume ya taifa ya uchaguzi
nchini Rwanda imesema imeliondoa jina la Diane Rwigara kwa kuwa hakukidhi
vigezo mbalimbali vinavyohitajika kama kuwasilisha nyaraka inayoonyesha
kutokuwa na rekodi ya uhalifu, kushindwa kutoa hati inayothibitisha kuwa ana
asili ya Rwanda na pia kukusanya jumla ya saini 600 za uungwaji mkono zikiwemo
12 kutoka wilaya nane.
Rwigara alienguliwa
katika uchaguzi wa mwaka 2017 kwa tuhuma za kughushi saini za wafuasi wake.
Alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa hilo pamoja na kuchochea uasi huku akizuiliwa
kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuachiliwa huru baada ya kutokutwa na hatia
mnamo mwaka 2018.
Kagame, amekuwa na
ushawishi mkubwa nchini Rwanda tangu yalipomalizika mauaji ya kimbari ya mwaka
1994 ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 800,000 wengi wao wakiwa
ni watutsi.
Rais Kagame amekuwa rais
wa taifa hilo dogo la Afrika Mashariki tangu mwaka 2000 na ameshinda chaguzi
tatu kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura na bila shaka anatarajiwa kushinda tena
mwezi Julai. Kiongozi huyo amekuwa akisifiwa kwa kuijenga upya Rwanda lakini
mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaishutumu serikali yake kwa vitendo
vya ukiukwaji mkubwa wa kuukandamiza upinzani.
Rwanda itafanya uchaguzi
wa rais na wabunge Julai 15 baada ya serikali kuamua mwaka jana kuoanisha
tarehe za chaguzi hizo.