MASHIRIKA ya kutetea haki za wafanyakazi ya Nigeria yameizima gridi ya kitaifa ya umeme nchini humo na kutatiza usafiri wa ndege jana.
Haya yamefanyika baada ya
mashirika hayo kuanzisha mgomo uliosababisha kufungwa kwa shule na afisi za
umma baada ya kushindwa kufikia maelewano na serikali kuhusiana na mshahara wa
chini kabisa wanaostahili kulipwa wafanyakazi.
Mashirika hayo mawili
makuu, Nigeria Labour Congress NLC na Trade Union Congress TUC yamesema
yamewaamrisha wanachama wake kususia kazi baada ya serikali kukataa kuongeza
mshahara wa chini zaidi kuwa zaidi ya dola 40 kwa mwezi.
Serikali ya nchi hiyo
imechapisha taarifa ikisema ina nia ya kuongeza mshahara huo wa chini kabisa na
kwamba itafanya mazungumzo na mashirika hayo kila siku kuhakikisha suluhu
linapatikana.
Afisi ya rais wa nchi
hiyo pia imetoa wito wa mkondo wa mazungumzo kufuatwa na pande zote mbili kwa
ajili ya kupatikana kwa mwafaka.