WADAU wa masuala ya saikolojia, wanasheria, wanazuoni na wanajamii wamebainisha sababu kadhaa zinazochangia ndoa kuvunjika mapema baada ya kufungwa, hususan mijini.
Wameeleza
hayo walipochangia mjadala wa Mwananchi X Space Jana Jumatano Septemba 18, 2024
ulioongozwa na mada isemayo: ‘Nini kinachochea ndoa zinazofungwa mijini
kuvunjika mapema?’
Mada katika
mjadala huo ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)
inatokana na ripoti ya hivi karibuni ya Chama cha Wanasheria wa Familia
inayoeleza ndoa zinazofungwa mijini kwa asilimia 40 zinavunjika chini ya miaka
mitano ya kwanza.
Nini sababu
ya mahusiano na ndoa za wengi kuvunjika?
Mwanachama
wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa), Jesusa Charles amesema miongoni
mwa yanayochangia ndoa kuvunjika mapema ni utandawazi.
“Utandawazi
umesababisha dunia kuwa kijiji na kuna mambo mengi yanayoendelea na yanatuzidi,
kadri yanavyotuzidi ndoa zinakuwa haziko salama. Watu wanashidana na kuondoka
katika uhalisia wao.
“Unaweza
kujikuta upo kwenye mahusiano mtu anaangalia mtu mwingine anafanya nini, mtindo
huo unapoendelea ina maana mtu unaanza kujikataa na kumuona mwenza wako hafai
sababu tu umeangalia mambo fulani katika mtandao,” amesema.
Mbali ya
hilo, amesema mambo wanayopitia watu yanaacha hisia, lakini vidonda hivyo huwa
havionekani, akitaja mfano wa unyanyasaji.
“Wengi
wanahisi wakiingia kwenye ndoa vitapona na wengi wanafanya hivyo wakiwa na
lengo la kujiweka sehemu salama, lakini unakuta kadri muda unavyoenda lengo
linashindwa kutimizwa mwisho wa siku mtu anakata tamaa,” amesema.
Kukosa
uvumilivu
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mjege Kinyota amesema matatizo ya ndoa
kama vile vipigo na usaliti si kwamba hayakuwepo zamani, bali kulikuwa na
uvumilivu na kuficha mambo yanayowakabili wanandoa.
Amesema
suala la kuachika lilikuwa aibu, tofauti na ilivyo sasa.
Dk Kinyota
amesema matarajio ya sasa kama vile mwenza wako akupatie kila kitu ni miongoni
mwa sababu za ugomvi katika ndoa.
“Una mume au
mke unataka kila kitu akupatie, na yeye unakuta yuko ‘bize’ anatafuta maisha
kwa hiyo lazima ugomvi uanze,” amesema.
Amesema
msingi wa ndoa unajengwa na mapenzi ya dhati kama ilivyokuwa zamani, lakini
siku hizi watu wanaoa na kuolewa kwa sababu ya kipato na mali na si msingi wa
mapenzi ya kweli.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla),
Tike Mwambipile amesema sheria ya ndoa inaelekeza mwanamume akiwa ameoa lazima
awajibike kumtunza mke.
Hata hivyo,
inapotokea sababu maalumu kama kuumwa au hana kazi, basi mkewe ana wajibu wa
kisheria kumtunza mume wake.
Amesema kwa
sasa wanawake wana vipato kutokana na masuala ya usawa wa kijinsia na wakati
mwingine mke ana kipato kumzidi mume wake, lakini changamoto hutokea kutokana na
kutokuwa na uelewa kati yao.
“Suala
lililopo ni kutafakari kwa namna gani tunaweza kusaidiana katika hili. Lakini
kikubwa mwanaume ili apate heshima yake vizuri, basi anapaswa atunze familia
hata kama mkewe ana kipato,” amesema.
Tamaduni
kandamizi
Tamaduni
zisizotoa usawa kwa wanawake na wanaume imeelezwa huchangia ndoa kuvunjika.
Joseph
Wasira, akichangia mjadala huo amesema katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa
ndoa kuvunjika huchangiwa na tamaduni kandamizi zisizotoa usawa kwa mwanamke na
mwanaume.
“Wanawake wa
maeneo hayo wameanza kupata mwanga kwa kutambua walikuwa wanapata mateso,
wanaamua kuacha ndoa kwenda kutafuta maisha mapya kwa sababu tu ya kukosekana
uwiano wa usawa,” amesema.
Wasira
amesema ukilinganisha ukubwa wa tatizo hilo, vijijini ni kubwa zaidi kuliko
mijini na taasisi za kiraia zimekuwa zikienda maeneo hayo kutoa elimu.
Amesema
usasa pia unaathiri taasisi ya ndoa, akisema maadili yameporomoka, hivyo watu
hawaoni umuhimu wa kuwa ndani ya ndoa kama ilivyokuwa zamani.
Wasira
amesema pia ndoa za mijini huvunjika kutokana na familia kutokuwaanda vijana
katika malezi.
Mbali ya
hayo, imeelezwa umaskini wa fikra na uwepo wa matatizo ya afya ya akili
kutokana na mfumo wa maisha uliopo mijini, kulinganisha na vijijini ni miongoni
mwa sababu za kuvunjika mapema kwa ndoa za mijini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Akili Platform Tanzania, Roghat Robert amesema mengine
yanayochangia kuvunjika ndoa za mijini ni umbea, kusambaza uvumi, taarifa
zisizo za kweli, makundi na mtazamo uliopo kwa baadhi ya watu kwamba mtu
akishapata pesa anabadilika.
“Tulifanya
dodoso tukagundua ukichukua wadada 10 ukiwauliza wanasema wanatamani kuzaa,
lakini hawataki kuwa chini ya mwanaume, hivyo unagundua wengi wanajikuta
wakikata tamaa kutokana na mfumo wa maisha na matukio yanayotokea,” amesema.
Ni nini
kifanyike, amesema lazima watu waandaliwe mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa,
ili watakapoingia wajue majukumu yao na kuvumilia upungufu wa kila mmoja.
Matarajio
makubwa
Kenny Mmari
akichangia mjadala huo amesema matarajio makubwa yasiyokuwa na uhalisia ni chanzo
cha ndoa kuvunjika mapema.
Amesema,
“watu wanachukulia wanavyoviona kwenye vyombo vya habari na katika filamu,
wanaingia na matarajio hayo, sasa wakiingia wakikutana na mambo tofauti
wanaachana.
“Mijini ni
mfano mzuri wa utandawazi kuliko vijijini, yanayotokea kwenye miji ya Tanzania
na Afrika na sehemu zingine duniani ni kiashiria ya kile kinachotokea maeneo
yote.”
Mmari
ametaja sababu nyingine ni mabadiliko ya wajibu wa kijinsia akisema,
"zamani tamadani zetu zilikuwa zinamfanya mwanamke kuwa na watoto na kuwa
mtu wa nyumbani, lakini leo wana uhuru zaidi si jambo baya lakini inasababisha
migogoro ya kuvunjika ndoa.”
Amesema
kadri ustaarabu wa binadamu unavyopiga hatua unasababisha kila mtu kutafuta
utimilifu wa haki yake na kupata furaha itakayomfanya afurahie maisha.
“Mahitaji hayo
yanapoongezeka yanasababisha mgongano wa masilahi na ilivyo mjini watu wengi
wamebadilika na kuzoea utamaduni wa kidunia zaidi kuliko wa vijijini,” amesema.
Mali badala
ya upendo
Ndoa
zinazojengwa katika misingi ya mali badala ya upendo pia zimetajwa kuvunjika
mapema.
“Ustawi wa
Taifa unategemea ustawi wa mahusiano ya ndoa na familia kwa ujumla, kukosekana
kwa msingi mzuri wengi wanapuuza. Miaka ya nyuma vijijini msingi wa ndoa ilikuwa
watu kukutana na kupendana na kuamua kuoana.
“Mapenzi
yalikuwa msingi wenyewe, mambo yanavyobadilika watu wanakengeuka, ule utaratibu
wa zamani mfano mtu anaweza kuwa na mtu wake anampenda lakini akaona bado
anapambana na maisha anamfuata aliyefanikiwa kimaisha,” amesema Hemed Tawa
akichangia mjadala huo.
Amesema
vijana wengi wanaangalia mtu aliyefanikiwa au kuwa na kazi wakiamini hata kuwa
mzigo katika maisha yake bila kujali kama anampenda.
“Matokeo
yake tunatoka kwenye msingi halisia ambao ungeisimamisha ndoa na kustawi. Kwa
hiyo mnakuwa matapeli wawili mmekutana kila mmoja kaja na sababu yake lakini
wanashindwa kuambiana,” amesema.
Awali,
akichokoza mada, Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Kalunde Jamal amesema kukosa
elimu ya ndao kwa walio wengi nchini ni sababu ya nyingi zinazofungwa kuvunjika
ndani ya muda mfupi.
“Tatizo liko
maeneo yote mijini na vijijini, inaweza kuwa mijini hali imezidi.
Nilichokigundua hakuna elimu ya ndoa, walio wengi wanaingia kama fasheni,
hawajui wanaenda kukutana na nini kwa wanaume na wanawake,” amesema.
Amesema
tatizo lingine ni usasa, akieleza kutokana na mabadiliko ya teknolojia mtu
anakuwa na uwanja mpana wa kujifunza mambo kwa kusikiliza wanachozungumza wengine
kupitia mitandao ya kijamii.
Kuhusu
takwimu
Ripoti ya
matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonyesha takwimu za watu
kupeana talaka zimeongezeka zaidi ya mara nne ikilinganisha na sensa ya mwaka
2012.
Mkuu wa
Dawati la Takwimu katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL),
Halili Letea amesema, “kiwango cha talaka kwa mwaka 2022 ilikuwa asilimia 3.7
ikilinganishwa na asilimia 0.9 mwaka 2012. Hivyo kuna ongezeko la wanaoachana.
Pia wapo waliotengana bila talaka walikuwa asilimia 1.8 mwaka 2022 tofauti na
asilimia 2.9 mwaka 2012.”
JISAJIRI SASA NA PLAY
MASTER BET - BETI KIRAHISI
BONYEZA HAPA KUJISAJIRI