KAMA
ulidhani kuzaliwa kwako na baba na mama kunakupa uhalali usio na shaka wa
kurithi mali walizonazo unakosea, lipo takwa la kisheria linalokuondolea haki
hiyo, ingawa mwenye mali ni baba au mama yako wa damu.
Pengine
huu unaweza kuwa ukweli mchungu kwa baadhi ya warithi, kutokana na uhalisia wa
matukio kadhaa ya ugomvi wa mali za urithi yanayozikabili familia mbalimbali na
wengine kufikia hatua ya kukatizana uhai.
Mfano
wa hayo ni familia ya Bwire Mathayo ya Kibaha mkoani Pwani, iliyoingia kwenye
mzozo wa mirathi, baada ya mama yao kufariki dunia na kuacha mali.
Mzozo
huo umetokana na wakubwa kugoma kuwaingiza wadogo zao kwenye mirathi, wakidai
hawastahili kwa kuwa mali hizo zilichumwa na baba yao.
Katika
familia hiyo, Justine Zuberi alidai baba aliyefariki dunia, ndiye mmiliki wa
mali hizo na si baba yao wa kambo (Bwire Mathayo) aliyemuoa mama yao na kumkuta
na mali alizoachiwa na baba yao.
Mama
yao huyo alifariki dunia Desemba 2023 na kuacha watoto wanne, lakini kwa baba
wawili tofauti.
Binti
mdogo, Sabrina Mathayo anasema mgogoro huo umeigawa familia, haina maelewano,
baadhi ya wanandugu wanaamini watoto wote wana haki ya kupata urithi kwa mama
yao, kwani wote ni watoto wa marehemu na wengine wanapinga.
Mkasa
mwingine unaikabili familia mjini Morogoro, baada ya baba kufariki dunia, mmoja
wa watoto wake aliingia kwenye mgogoro na wenzake akipinga kuenguliwa kwenye
mirathi.
Kijana
huyo, Deniss Joachim (sio jina lake halisi) anataka kuwa mmoja wa warithi,
ndugu zake wanagoma wakisisitiza baba yao akiwa hai alimuengua kwenye warithi
wake na wosia aliouacha umebainisha hilo.
Kama
hiyo haitoshi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alieleza mgogoro wa
mirathi wa watoto wa familia moja mkoani humo waliokwenda ofisini kwake kutaka
usuluhishi.
Katika
mgogoro huo, watoto wadogo watatu walipinga wakubwa zao wawili kuwa wasimamizi
wa mirathi, wakitoa hoja kuwa ndugu zao hawakutaka baba yao apelekwe hospitali
alipougua, iweje afariki dunia ndiyo wawe wasiwamizi wa mirathi yake.
Katika
simulizi hiyo, Mtaka alisema wale wadogo walipoulizwa kwanini hawataki kaka zao
wasimamie mirathi, wakasema baba yao alipata kiharusi, waliposhauri apelekwe
Muhimbili (Hospital ya Taifa jijini Dar es Salaam), wale wakubwa walikataa
wakidai mzazi wao huyo anaweza kufa muda wowote.
“Alikaa
kwenye hali ya ugonjwa mwaka mmoja na miezi minne na kufariki, mvutano
ulikuwa wadogo hawataki kaka zao kuwa wasimamizi wa mirathi, wakitoa hoja
kwamba ndugu zao walikataa baba yao asipelekwe Muhimbili kwa matibabu zaidi,
wakati pesa ambazo zingetumika zilikuwa zake, wakidai walitaka afe ili wagawane
fedha za baba yao zikiwa nyingi.
“Wakubwa
nilipowauliza wakasema mzee wao alikuwa amefikia kwenye koma, hivyo huenda
angefia njiani, lakini swali la kujiuliza hata kama wangechukua ambulance
wakalipa milioni 80, hela ni ya mgonjwa mwenyewe,” alisema Mtaka.
Ufafanuzi
wa kisheria
Akizungumzia
sintofahamu hiyo, Ofisa Usajili wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini
(Rita), Joseph Mwakatobe anasema kuna vigezo vinavyomuondoa mtoto kwenye
mirathi iwe baba/mama yake aliacha wosia au la.
“Kwa
aliyeacha wosia, mwenye mali anaweza asimrithishe mtoto wake, lakini ni lazima
amtaje kuwa ni miongoni mwa watoto wake na sababu za kutomuweka kwenye orodha
ya warithi wake na ziwe na ushahidi,” anasema.
Kwa
ambaye hakuacha wosia, anasema lazima kuwepo na mashahidi wasiopungua wanne
kuthibitisha hilo kuwa mtoto husika hastahili kurithi na Mahakama itaviangalia
kama vya msingi.
Kinachomuondolea
mtoto uhalali wa kurithi
Pamoja
na sababu nyingine, hatua ya kuzini na mke au mume na muandika wosia ni moja ya
vigezo vinavyomwondolea mtoto haki ya kurithi.
“Hilo
likithibitika, linamuondoa mtoto huyo katika haki hiyo kwa kuwa ni mkosefu wa
maadili,” anasema.
Kama
wewe ni mtoto na unaharibu mali za mzazi wako, hesabu hiyo ni moja ya sababu
zinazokuondolea sifa ya kurithi kwa mujibu wa Mwakatobe.
“Mali
aliyoharibu ndiyo itahesabika kuwa ni urithi wake, mzazi akiandika au hata
kutamka na ndugu jamaa wakawa wanafahamu, hiyo ni moja ya vigezo vinavyomuondoa
huyo mtoto katika mirathi,” anasema.
Lakini,
ukishindwa kutoa huduma kwa mzazi wao angali hai, anasema ni sababu nyingine
inayokuondolea sifa ya kumrithi.
“Ni
kweli huyo mwanao ni mrithi wako, lakini hakukujali labda wakati unaumwa, hiyo
inapelekea dhana kwamba pengine anataka ufe ili arithi, na baadhi ya mifano ipo
watoto wengine huwaombea mabaya wazazi wao, ili tu warithi mali, kigezo hicho
kikiwa na ushahidi kinakuondoa kwenye mirithi,” anasema.
Lakini,
anasema mtoto anaweza kupinga mahakamani kama mzazi ameacha wosia na Mahakama
itaangalia kama vigezo vilizingatiwa.
Mama
mwenye watoto wa baba tofauti
Akifafanua
mirathi ya watoto waliochangia mama, Mwakatobe anasema kama mume wa kwanza wa
mama huyo alipofariki dunia ulifanyika mgao na kila mmoja (mke na watoto), mama
huyo akifariki watoto na mume wake mpya atakuwa na haki ya kumrithi.
“Kama
mgao ulifanyika mume wake wa kwanza alipofariki, inamaanisha watoto wakubwa
tayari walishapata mgao wao, na kama haukufanyika mali zote zikaenda kwa mama
hiyo ni utaratibu anapaswa kufanya mgao bila kuangalia alizaa na nani.
“Mwakatobe
anasema kuna migogoro watoto wakubwa wanadai mali alichuma baba yao, lakini
kama mali hizo ziligawanywa baba wa kwanza alipofariki, kisha baadaye mama
akaolewa na kuzaa, ikitokea huyo mama amefariki wote ni uzao wa tumbo lake na
kila mtoto anastahili kurithi na hata huyo mume aliyekuwa amemuoa naye
anastahili,” anasema.
Anasema
huyo mama akiwa na hekima atawaweka wazi mapema kuhusu mali zake na kueleza
hizo mali alichuma na baba gani na warithi wake ni watoto wake na wale wa baba
mwingine ataangalia baba yao na mali zao.
“Kama
hakufanya hivyo, hakuacha wosia na hakuna maandishi na nyaraka, basi vyote
vinakwenda kwa wale warithi wake hata mume aliyekuwa amemuoa anaweza kurithi,
kwani anapofariki mwenye mali zake, mali zitangukia kwa warithi wake,” anasema.
Wajukuu
wanaweza kurithi?
Mwakatobe
anasema katika sheria wanaopaswa kurithi ni wale walioachwa na marehemu, mke,
mume, wazazi au watoto.
"Kama
watoto wa huyo marehemu walitangulia kabla ya baba yao, lakini nao wameacha
watoto (wajukuu wa marehemu) hao hawana nafasi labda kama awe aliacha wosia na
kuwaandika kwenye mirathi.
"Kinyume
na hapo, hao wajukuu tunasema baba au mama yao alikimbia urithi, kwa sababu
walifariki kabla ya mwenye mali na ikitokea wamepata basi ni busara tu
inatumika kwenye familia,” anasema.
Unavyoweza
kuandika Wosia
Mwakatobe
anasema, ili kuandika wosia unakwenda Rita kwanza ukiwa peke yako.
"Haihitaji
kitu kingine zaidi ya kuja wewe kama wewe, tutakuelekeza, utaandika mali zako
na sisi tutakupangia tarehe ambayo utakuja na mashahidi wawili, ili kuandika
wosia," anasema.
Hata
hivyo, Mwakatobe anasema kitu cha muhimu ambacho watu wanapaswa kukifahamu ni
kwamba kuandika wosia inaweza isiwe kigezo cha usimamizi wa mirathi yako pale
unapokuwa umefariki endapo wosia utakosa vigezo.
"Hii
imekua ikileta shida, unaweza kujiuliza inakuwaje Mahakama imekataa wosia na
marehemu aliuandika akiwa hai? Ndiyo anaweza kuwa ameandika, lakini haujakidhi
vigezo, sisi Rita kabla ya kuandika tunakupa elimu kwanza," anasema.
Anasema
kwenye wosia mbali na mali, unaandika pia madeni na lazima uwaorodheshe watoto
wako na kama miongoni mwao yupo ambaye humpi urithi na ueleze sababu na umtaje
msimamizi wa mirathi.
"Unapokuja
kuandika wosia uthibitisho wa mali zako unao mwenyewe, Rita tunachohitaji ni
taarifa na taarifa yako anakua nayo kichwani, kama una vitu vingi, tunakwambia
kaa tulia andika summary ya vitu vyako.
"Wosia
unaweza kukosa vigezo, kama muandikaji ameandika si kwa hiari yake, kwani kuna
watoto huwa wanalazimisha baba aandike, kisa labda kaoa mke mwingine halafu
wanaona hizo mali zilichumwa na mama yao," anaeleza.
Anasema
kigezo cha kwanza katika kuandika wosia lazima uwe na hiari nao, pili ni
utimilifu wa akili ukijua kile unachoandika na unakikumbuka.
"Pia
uwe na mashahidi wasiopungua wawili na lazima uchapwe, usifutwe futwe na
kilichoandikwa kisilete utata na usainiwe na muandikaji na mashahidi siku moja
na uthibitishwe,” anasema.
Anasema
kwenye wosia shahidi anaweza kufariki dunia kabla ya mwenye mali, hivyo wosia
unaweza kubadilika mara kwa mara kulingana na uhitaji uliopo.
Kwa
mujibu wa Mwakatobe, gharama za kuandika wosia zinaanzia Sh30,000 na kuuhifadhi
ni Sh30,000 kwa mali isiyozidi Sh50 milioni.
Kuanzia
mali za Sh50 milioni hadi Sh500 milioni kuandika ni Sh100,000 na kuuhifadhi ni
Sh100,000.
Kwa
mali ya kuanzia Sh500 milioni na zaidi kuandika ni Sh150,000 na kuuhifadhi ni
Sh150,000.
"Mali
hizo huwa tunazifanyia makadirio na kutathimini kulingana na mazingira,"
anasema.
JISAJIRI SASA NA PLAY
MASTER BET - BETI KIRAHISI
BONYEZA HAPA KUJISAJIRI